Habari

Imewekwa: Jan, 29 2020

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA MHANDISI STELLA MANYANYA AKIZINDUA MASHINE YA KUCHAKATA ZABIBU.

News Images

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Mhandisi STELLA MANYANYA (Mb), amesema kunahaja ya kuziwezesha kifedha taasisi za utafiti zinazobuni na kutekeleza teknolojia rahisi hapa nchini ili kufikia lengo la kuwa na viwanda na kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Naibu Waziri Manyanya ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizindua teknolojia mpya ya mashine ya kukamua mchuzi wa zao la zabibu katika kiwanda kidogo Cha WENDECHE kilichopo Kata ya Hombolo Bwawani, iliyobuniwa na TEMDO kwa kushirikiana na SIDO.

Alisema kuna haja ya kuziwezesha taasisi kama SIDO, TEMDO, CAMATEC, TIRDO na nyinginezo, kwani kwa muda mrefu taasisi hizo zilikuwepo lakini hazikuweza kunufaisha Watanzania. Lakini tangu zimewezeshwa kifedha tayari matokeo yameanza kuonekana.

"Hii inafurahisha sana hizi taasisi zimewezsshwa na matokeo chanya tumeyaona, "alisema Manyanya.

Alisema kuwezeshwa kwa taasisi hizi pia kumesaidia ukuaji wa viwanda nchini, na inatia moyo kuviwezesha zaidi..

Aidha alisema hakuna haja ya kubaki nyuma tunafanya kile tunachoweza na baadae kitaleta matokeo makubwa hapo baadae na kufikia Tanzania ya viwanda kama ilivyokusudiwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais John P. Magufuli.

Mbali na hilo Naibu Waziri Manyanya amewapa wiki tatu TEMDO kuhakikisha wanawatengenezea mashine wajasiriamali ambao walitoa oda ya kutengenezewa mashine hiyo ili nao waendelee na shughuli ya uchakataji wa zabibu kwani mashine hizo ni nzuri na zina ufanisi wa hali ya juu.

Alisema hakuna sababu ya kuwacheleweshea kwa sababu wanahitaji kwa ajili ya kufanya maendeleo.

Kwa upande wake Meneja Taasisi ya ubunifu na uhandisi Mitambo, TEMDO, Mhandisi Alexander Komba, alisema kazi yao ni kubuni na kuendeleza Technolojia kwa ajili ya wajasiliamali wazalishaji, kisha kupeleka kwa SIDO ili ziweze kuwafikia walengwa. Kutokana na ushirikiano huo taasisi hizo mbili ambazo ziko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, waliweza kutatua changamoto ya kuchakata zao la Zabibu kwa haraka.